Mabadiliko Forums

Log in Register

Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *

Deo Filikunjombe, Capt. Slaa wafariki; Ni kwa ajali ya Helkopta 5Y DKK

Chopa iliyopata ajaliDAR ES SALAAM: Aliyekuwa Mgombea wa Ubunge Jimbo la Ludewa kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi, Deo Filikunjombe na watu wengine watatu wamepoteza maisha katika ajali ya Helkopta iliyotokea Oktoba 15 mwaka huu usiku katika eneo la Hifadhi ya Selous.

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, amesema chopa hiyo ilikuwa imebeba abiria wanne wakitokea Dar es Salaam kwenda mkoani Njombe na kwamba waliotambuliwa hadi sasa ni rubani wa chopa hiyo Capt. William Slaa, na Deo Filikunjombe.

Kwa mujibu wa Chagonja, uchunguzi wa Helkopta hiyo yenye namba 5YDDK unaendelea na kuwa abiria wengine wawili bado hawajatambulika majina yao.

Kifo cha Filikunjombe kinafanya idadi ya wagombea ubunge waliofariki kabla ya uchaguzi mkuu kufikia 6, akiwemo, Mohamed Mtoi (CHADEMA), Emmanuel Makaidi (NLD),Daktari Abdallah Kidoda (CCM), Estomii Malla (ACT Wazalendo), pamoja na Selina Kombani (CCM).

Meya wa Ilala, Jerry Silaa aliandika kwenye ukurasa wake wa Istagram kuwa “Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa rasmi kutoka kwa timu ya uokoaji imefanikiwa kufika eneo la ajali na kukuta abiria wote na rubani wamepoteza maisha”.

Taarifa yake iliendelea kueleza, “Nimepoteza Baba na rubani mzuri wa nchi yetu Capt. William Silaa, nimepoteza rafiki na kiongozi wangu, Deo Filikunjombe. Nawapa pole wote waliopoteza ndugu zao. Nawaombea marehemu mapumziko ya Amani. Nawashukuru wote walioshirikiana na familia kusaidia uokozi”.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu amekaririwa na vyombo vya habari akithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema Helkopta hiyo imedondoka katika hifadhi hiyo katika Kitalu R3 na watu walioshuhudia tukio hilo walikuwa Kitalu R2.

Tangu kuripotiwa kwa tukio hilo, kulikuwa na utata wa hali ya abiria wanne na rubani waliokuwa ndani ya chopa hiyo. Taarifa hizo zilianza kusambaa katika mitandao ya kijamii jana usiku zilieleza kuwa helkopta hiyo ilikuwa na watu wanne na rubani mmoja.

Filikunjombe ndiye aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya PAC, iliyofanya kazi mbalimbali ikiwemo kuchunguza ufisadi kuhusu Fedha za Akaunti ya Escrow wa zaidi ya Sh. bilioni 300 ambayo ripoti yao ilisababisha nchi kutikisika huku marehemu pamoja na baadhi ya wajumbe wa Kamati hiyo kudai kutishiwa maisha.

Ripoti ya Escrow ilisababisha aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Professa Sospeter Muhongo kujiuzulu na aliyekuwa Katibu Mkuu Eliachim Maswi kusimamishwa Kazi kupishwa uchunguzi wa tuhuma hizo.

Baada ya muda Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, alitoa ripoti ya uchunguzi na kumsafisha Maswi na Professa Muhongo Kuwa hawana hatia.

Marehemu alizaliwa mwaka 1972, alisoma shule ya Msingi ya Ludewa mwaka 1986, alisoma pia katika Sule ya Seminari ya Kasita Dayosisi ya Mahenge 1989-1992, baadae alisoma katika Shule ya Sekondari Forest Hill Morogoro kati ya mwaka 1994 na 1996.

Kati ya mwaka 1996 na 1999 alisoma katika Chuo Kikuu Cha Marerere kilichopo Kampala, Uganda Elimu ya Mawasiliano ya Umma, Shahada ya Uzamili. Pia alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Fedha za Serikali wilayani humo, tangu mwaka 2006 na mwanachama wa Kamati ya Siasa mkoa wa Njombe hadi mauti yalipomkuta.

Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, John Magufuli, ametuma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga, kutokana kifo hicho.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Chama hicho, Ofisi Ndogo ya Lumumba, Jijini Dar es Salaam, imesema Magufuli, ambaye pia ni Mbunge anayemaliza muda wake wa Jimbo la Chato na Waziri wa Miundombinu, ametuma pia salamu za rambirambi kwa kada maarufu na Meya wa Manispaa ya Ilala, Jerry Silaa ambaye amefiwa na baba yake mzazi, Capt. William Slaa ambaye alikuwa rubani wa helkopta hiyo.

Source: Fikra Pevu.

Add comment


Security code


Refresh