Mabadiliko Forums

Log in Register

Login to your account

Username *
Password *
Remember Me

Create an account

Fields marked with an asterisk (*) are required.
Name *
Username *
Password *
Verify password *
Email *
Verify email *

MWANZA: Jeshi Polisi Mkoa wa Mwanza limetangaza kuwashikilia watu wanne kwa kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja akiwemo mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGM) Milembe Selemani na Janeth Shonza ambao watafikisha mahakamani hivi karibuni.

Akizungumza na Mabadiliko Forums, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alieleza kuwa watuhumiwa hao wanaotarajia kufikisha mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika ni Milembe Selemani (36), Janeth Julius Shonza (25) ambaye ni maarufu kwa jina la Double J, aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha St. Augustino (SAUT) Mwanza na Aneth William Mkuki wote wakazi wa mtaa wa Nyasaka Jijini Mwanza.

Alimtaja mtuhumiwa mwingine kwamba ni Richard Fabian (28) maarufu kwa jina la Rich Mavoko, mkazi wa Buzuruga ambaye yeye anatuhumiwa kwa kosa la kusambaza video iliyokuwa ikimuonyesha Milembe maarufu kama Kim the Don akimvisha pete ya uchumba aliyedaiwa kuwa mpenzi wake Janeth Julius Shonza kwenye mitandao ya kijamii kitendo ambacho ni kinyume na sheria.

“Mnamo Novemba 32, mwaka huu majira ya saa 5:00 usiku katika kata na Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, watu hawa wakiwa katika hoteli ya Pentagon Jijini Mwanza waliandaa tafrija ndogo kwa ajili ya kuvishana pete ya uchumba na kurekodi video yake ambayo ilirushwa kwenye mitandao ya kijamii.

“Baada ya kipande hicho cha video kuonesha mwanamke mmoja akijifanya kama mwanaume akimvisha pete ya uchumba mpenzi wake huku watu wengine waliokuwepo kwenye sherehe hiyo wakishangilia na kuwapongeza, polisi tulianza kuwasaka wahusika katika maeno yote ya jiji  mkoani Mwanza na maeneo ya mikoa ya jirani,” alisema.

Alisema msako wao ulifanikiwa kumkamata Milembe Suleimani mkoani Geita ambae alionenekana kwenye video akimvisha pete mwenzake na baadae polisi walimnasa mpenzi wake Janeth akiwa mkoani Singida.

Katika ufuatiliaji wa kina pia walifanikiwa kuwakamata Aneth Wiliam Mkuki ambae pia anadaiwa kujihusisha katika mapenzi ya jinsia moja na Janeth ambae alitoroka nae hadi Singida kisha kumkamata Richard Fabian aliyesambaza video hizo kwenye mitandao ya kijamii.

“Sasa baada ya kuwakamata hawa watu katika mahojiano ya awali watuhumiwa wote walikiri kuwa ni kweli walifanya sherehe hiyo Novemba 31 mwaka huu saa 5 usiku katika ukumbi wa Pentagone hotel uliopo mtaa wa Rwagasore wilayani Nyamagana na kurekodi video iliowaonesha wakivishana pete,” alisisitiza.

Kamanda Msangi alisema bado pilisi wanaendelea na mahojiano baada ya kuwakamata watuhumiwa wote ikiwa ni pamoja na kuwatafuta watu wengine walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika shughuli hiyo na mara baada ya kukamilika kwa uchunguzi watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

wanaendelea na mahojiano na watuhumiwa wote na pia kuwatafuta watu wengine walioshiriki kwa namna moja au nyingine katika shauri hili, pindi uchunguzi ukikamilika watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani.

DAR ES SALAAM: Aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Anna Mghwira na baadaye kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ametangaza rasmi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akihutubia katika mkutano wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake CCM (UWT), Anna Mghwira alisema akiwa mwenyekiti wa ACT alipenda CCM walivyokuwa wakipanga mambo yao kwa kuelewana na kutanguliza maslai ya umma kwa ujumla.

“Naiona CCM inayokataa rushwa, inayotanguliza maslahi ya Taifa mbele chini ya uongozi wa Jemedari mahiri, Dk John Magufuli na sidhani kama kuna mtu atapenda kubaki nyuma kwani ameirudisha hadhi na heshima ilikuyokuwepo ndani ya Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla,” alisema.

Aidha alibainisha kuwa akiwa kama Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro licha ya kujiunga na CCM alihaidi kushirikiana na vyama vyote ikiwemo CHADEMA na NCCR ambavyo alidai ni vikubwa mkoani kwake lakini kusisitia kuwa CCM ndicho alichoona kinachobadilika.

Alisema ni kweli anaona juhudi za kila mtu lakini juhudi za mtu anaebadilika huwa ziko tofauti na kutoa mfano wa mtu alieokoka kuwa huwa haami duniani bali anatoa taarifa kuwa amebadilika na anataka kuwa mtu bora zaidi.

“Baada ya kufanya kazi chini ya serikali kwa takribani miezi sita, nimeona ninazo sababu za kutangaza  kujiungana na Chama Cha Mapinduzi na najiungana na kina mama wenzangu wanaotaka kubadilika, kupambana na kutoa muda wao wa thamani kuhakikisha Taifa linakuwa mahali salama kuishi na mfano wa kulea jamii, kizalendo na kiuajibikaji,” alisema.

Anna Mghwira anakuwa kiongozi wa nne kujiengua katika chama hicho na kujiunga na CCM, wakwanza akiwa ni Samson Mwigamba aliyetangaza kujiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Kampeni na Uchaguzi Taifa na ujumbe wa Kamati Kuu ya ACT Wazalendo, Oktoba 16,2017 na baadaye kujiunga chama hicho.

Mwingine ni Profesa Kitila Mkumbo ambaye pia alitangaza kujiunga na CCM Novemba 17, mwaka huu na kutangaza na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida, Martha Mlata na baadaye kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Magufuli.

Uamuzi wa Prof. Kitila kujiunga CCM ni sawa na ule wa Anna Mghwira kwani yamefanyika baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagilia Rais Magufuli Aprili 4, mwaka huu na mwenzie akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Juni 3, mwaka huu.

Mwingine ni Wakili Albert Msando ambaye pia alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Ushauri wa Chama hicho Mei 23, mwaka huu lakini baadaye Novemba 21, mwaka huu kutangaza kujiunga na CCM na kufuatiwa na jana Wilson Elias Mwambe, ambaye ni Katibu wa kamati ya maadili mkoa wa Kigoma naye alitangaza kujiengua chama hicho pia.

Ajali ya Moto KaragweKARAGWE: Moto mkubwa umezuka na kuteketeza vibanda vya maduka zaidi ya 150 katika mji wa Kayanga wilaya ya Karagwe mkoa wa Kagera magharibi mwa Tanzania. Moto huo ambao ulianza Jumatatu majira ya sa 2:00 usiku umeteketeza mali na bidhaa za aina mbalimbali kama mchele, sukari, nguo, simu, pamoja na bidhaa zingine.

Gloria Kilio ambaye alikuwa akiuza vyakula vya nafaka, amesema stoo zake zote tatu (3) za nafaka zimeungua, “Stoo zilikuwa na magunia ya unga, mchele na sukari lakini vyote vimeteketea,” amesema Gloria huku akilia. Anasema wakati moto unatokea alikuwa tayari amekwisha kwenda nyumbani na kuwaacha wafanyakazi wake wakimalizia kufunga vibanda.

Wafanyabiashara wengi wanasema walikuwa na mikopo na wengi wao hawana bima ya mali zao. Jonasi Nyarugenda ni miongoni mwa wafanyabiashara hao: “Moto umeteketeza stoo zangu nne zenye bidhaa mbalimbali kama sukari, mchele, ngano na mafuta,: anasema Jonas na kuongeza, “kwakeli ukitathimini kwa haraka siyo chini ya milioni 45 zimepotea.” Amesema kwamba alikuwa hana bima katika mkopo wake wa milioni 20 kutoka katika benki.
Wafanyabiashara wamedai kupata hasara kutokana na ajali hiyo.

Hasara hiyo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na ukosefu wa vifaa vya kuzima moto. Wananchi wa Karagwe imewapasa kusubiri gari la Zimamoto kutoka Bukoba Mjini (magari ya uwanja wa ndege) ambako ni kilomita 120 kufika karagwe mjini. Hata hivyo magari hayo yalikuta maduka mengi yamekwishateketea.
Diwani wa kata ya Kanoni wilaya karagwe Sabi Rwazo amesema tukio hilo limewastua na ni tukio la kwanza la moto kuunguza soko wilayani humo. Anasema tatizo la ukosefu wa gari la zima moto linachangiwa na uhaba wa fedha. “Mara nyingi katika bajeti yetu imekuwa ikishindwa kununua gari.” Amesema Rwazo na kusema maombi yao yako serikali kuu.

Mkuu wa Wilaya ya Karagwe Deodatus Kinwiro amesema kuwa Serikali ya wilaya yake itapata gari la zima moto hivi karibuni, “Bahati nzuri nilikuwa Dar es Salaam, nimekutana na kamishna mkuu wa zima moto ameniahidi kunipatia gari jipya,” amesema Kinwiro na kuongeza kuwa, “wakati wowote gari hilo litafika wilayani Karagwe.”

Hata hivyo baadhi ya wananchi wanasema hawakubaliani na kauli hiyo ya mkuu wa wilaya kwa sababu wamekuwa wakitozwa kiasi cha TZS 30,000 kwa mwezi ili kuchangia huduma za zimamoto wilayani hapo lakini wanashangaa kwa nini hawapati elimu ya kujikinga na majanga, na hakuna hata gari la dharura.
Mpaka sasa chanzo cha moto huo hakijajulikana lakini taarifa za awali zimeonesha kuwa kuna Mamalishe mwenye kibanda sokoni hapo aliacha jiko lake bila kuzima hivyo likashika nguo zilizokuwa katika kibanda hicho na kusababisha moto kusambaa ghafla.

Msajili wa vyamaDAR ES SALAAM: Msajili wa Vyama vya Siasa nchini  Jaji Francis Mutungi ameviasa Vyama vya Siasa kushiriki chaguzi zinazotangazwa na tume za uchaguzi nchini ikiwemo uchaguzi wa Machi 20, mwaka 2016 uliotangazwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC).

Kauli hiyo ya Jaji Mtungi imetafsiriwa kuwa imelenga kukishawishi Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kimetangaza kutoshiriki uchaguzi wa marudio Zanzibar uliotangazwa na ZEC kufanyika Machi 20, mwaka huu.

 Kwa mujibu wa barua iliyotolewa  kwa vyama hivyo leo na kusainiwa na  Jaji Mutungi  ilieleza kwamba,  kimsingi Sheria ya Vyama Vya Siasa Sura ya 258 inasisitiza vyama vya siasa  kushiriki katika chaguzi zote zinazotangazwa na tume za uchaguzi ili kufikia malengo yake ya kushika dola.

“Katika nchi kidemokrasia na kwa chama cha siasa kinachoamini misingi ya kidemorasia ya vyama vingi vya siasa, hakuna njia mbadala kwa chama cha siasa kufikia malengo yake zaidi ya kushiriki uchaguzi.

“Ni wajibu wa kila chama cha siasa nchini  kama wakala wa kukuza demokrasia, utawala wa sheria na amani ya nchi, kuwa wa kwanza kutii matamko ya kisheria yanayotolewa na mamlaka  husika . Kama kuna chama cha siasa hakiridhiki au kimekwazwa kwa njia moja au nyingine na suala lolote kuhusu masuala ya uchaguzi, njia stahiki na inayonyesha ukomavu wa kisiasa si kuhamasisha kugomea uchaguzi, bali ni vema kikafuata utaratibu uliowekwa katika sheria za uchaguzi,” alisema Jaji Mutungi.

Aidha Msajili huyo amesema kwa mujibu wa Sheria za Nchi bado ni suala la hiari kwa chama kushiriki uchaguzi lakini utashi huo wa hiari unaenda sanjari na umuhimu wa kila chama kushiriki kila uchaguzi unaotangazwa na tume ya uchaguzi.

“Hivyo ni muhimu basi kila chama cha siasa kuelewa kuwa,uchaguzi ni kipimo cha uhai wa chama cha siasa. Chama cha siasa kisiposhiriki uchaguzi kinaua uhai wake katika mtazamo wa harakati za kisiasa,” alisisitiza.

Aliongeza kwamba hivi sasa, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi na vyama vya siasa vimeimarika, hivyo sio vyema kwa chama cha siasa kujirudisha nyuma au kujiua kisiasa kwa kutoshiriki uchaguzi wakati kina uwezo wa kufanya hivyo

MakabidhianoKAHAMA: Titmu ya Soka ya Ambasador FC kutoka wilayani Kahama mkoani Shinyanga inayoshiriki ligi daraja la pili ngazi ya mkoa wa Shinyanga imepokea  hundi ya Sh milioni 10.5 kutoka Kampuni ya madini ya Acacia kupitia mgodi wake wa Buzwagi.

Akizungumza jana katika makabidhiano ya hundi ya fedha hizo jana, Meneja mkuu wa mgodi huo Assa Mwaipopo alisema wameamua kuisaid atimu hiyo kutokana na kutinga hatua fainali ya michuano ya ligi daraja la pili ngazi ya mkoa wa Shinyanga huku akiwapongeza kwa kufanya vizuri.

Alisema kuwa msaada huo moja kati ya mikakati ya mgodi wa Buzwagi kuhakikisha inasaidia vikundi ama shughuli za kijamii a dhumuni la kutoa msaada kwa tim hiyo ambayo ipo katika wilaya ya Kahama ambapo ndipo mgodi huo unapofanyanyia shughuli zake za Madini.

“Lengo letu kubwa la kutoa msaada huu ni kutaka kuisaidia timu hii likiwa ni lengo la kutekeleza ahadi yetu ya kuisaidia jamii inayotuzunguka, kama mnakumbuka tumetoa udhamini kwa timu ya Stand Utd inayoshiriki lig kuu ya Vodacom na sasa tumetoa msaada huu wa fedha ili kuisaidia timu hii ifike mbali ifanye vizuri,” alisema Mwaipopo.

 “Hongereni kwa hatua mliyofikia, nimeelezwa kuwa mmefuzu kucheza fainali za mkoani, hiyo ni hatua nzuri ila naomba kuwasii viongozi, kuweni makini katika kuongoza timu yenu na mjitoe kuisadia timu na sio kufanya kazi kwa maslahi yenu binafsi kwakuwa timu imepata fedha hizo japo kidogo,”alisema Meneja.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa timu hiyo, Bakari Khalid akizungumza kwa niaba ya mkurungezi wa timu hiyo Aray Abeid, alii[ongeza kampuni hiyo na Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi kwa kuisaidia timu hiyo kwa kuwa fedha walizoepwa zitawasaidia maandalizi ya fainali za michuano hiyo na masuala mengine.

“Natoa shukrani kwa uongozi mzima Mgodi wa Buzwagi kwa ajili ya msaada huu, naomba kuaahidi kwamba sisi kama Ambassador tutafanya vizuri na kuitangaza Kahama katika sekta ya michezo kwani tunao vijana wazuri wenye uwezo wa kucheza mpira na kufanya hivi ni kukuza vipaji vya vijana wetu,”alisema Bakari.

Timu ya Ambasador FC inayofundishwa ipo chini ya Kocha wake Karume Songoro mchezaji wa zamani aliyewahi kuchezea vilabu vya Kahama Utd, Pamba ya Mwanza, Moro Utd ya Morogoro, Yanga na timu ya Taifa Stars.

TRL mabehewaMWANZA: Serikali imeeleza kuwa kuanzia leo Mkurugenzi mpya wa Shirika la Reli Tanzania (TRL) anatarajiwa kutangazwa ili kuanza kazi mara moja.

Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa TRL Mwanza, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa,  aliwaahidi wafanyakazi hao kumtangaza mkurugenzi mkuu wa pamoja na menejimenti mpya ya TRL kuanzia leo baada ya iliyokuwepo kuvunjwa.

Prof Mbarawa alisema Mkurungenzi huyo mpya anatarajiwa kutoka nje ya watumishi na watendaji wa shirika hilo kwa lengo la kuweza kuisaidia TRL ili liweze kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa na kuongeza mapato serikalini tofauti na sasa inavyojiendesha kwa hasara.

“Mkurugenzi mpya atatoka nje kabisa ya TRL  ili aweze  kuongeza ufanisi, kuisaidia pamoja na kuiwezesha TRL  kujiendesha kwa faida, mwaka mmoja na nusu sasa umepita serikali imewekeza fedha nyingi katika shirika hili na miundo mbinu yake  lakini hamna faida yoyote au mapato serikali inayoyapata  kutoka katika shirika hili,” alisema Prof. Mbarawa.

Hata hivyo Mbarawa alisema  upelelezi wa kesi ya udhaifu ulioainishwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), katika michakato ya zabuni mbili za manunuzi ya mabehewa 25  umekamilika na wakati wowote waliohusika watafikishwa mahakamani na ikibainika walihusika watafukuzwa kazi.

Awali baadhi ya wafanyakazi wa TRL walimweleza waziri matatizo mbalimbali yanayowakabili  likiwemo la malimbikizo ya mshahara,  madai ya fedha za kujikimu, kutopandishwa madaraja kwa muda mrefu pamoja na kutokuwasilishwa kwa michango yao katika mifuko ya hifadhi ya jamii tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

Pia wafanyakazi hao walimuomba Prof. Mbarawa  mkurugenzi mpya atakayetangazwa asifanye kazi na Kampuni Hodhi ya Rasilimali za reli Tanzania (RAHCO)  ambapo waziri huyo aliwaeleza kuwa kazi ya kampuni hiyo  imekwisha na wizara inatarajia  kuiunganisha na TRL.

Rais Magufuli akiwa kwenye Gwanda la JeshiARUSHA: Kuonekana kwa Rais Dk John Pombe Magufuli akiwa amevalia Gwanda za Jeshi kumukuwa ngumzo huku baadhi ya wachambuzi wa mambo wakikosoa hatua hiyo ya kutokuonyesha cheo chochote wakati akiwa ni Amiri Jeshi Mkuu.

Wakosoaji hao, walitolea mfano na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na kuweka picha zake akiwa amevalia Gwanda za jeshi la nchi yake huku zikiwa na cheo cha ‘Field Marshall’ na kusema muonekano wa Rais Magufuli umemfanya kuwa askari asiye na cheo.

Hata hivyo kutokna na mjadala huo kushamiri katika mitandao, watalaamu wa masuala ya Kijeshi ambao hawakupendwa kuandikwa majina yao, wametoa ufafanunuzi ufuatao juu ya hatua ya Rais Magufuli kuvalia Gwanda zisizo na cheo.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa mpaka sasa, Rais Magufuli atakuwa Rais wa pili baada ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuvalia gwanda za kijeshi huko nyuma na hata wakati wa Vita ya Uganda, lakini pia hakuwahi kuvalia zenye cheo.

Aidha, walieleza kuwa Jeshi ni taasisi ambayo imejengwa kwenye mifumo, sheria, miongozo na taratibu imara ambazo hazipaswi kuingiliana na mifumo ya kisiasa ikizingatiwa kuwa vyeo vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni lazima vitokane na mafunzo na elimu ya utumishi husika.

Wachambuaji hao walitoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete ambaye aliwahi kuwa mwanajeshi wa cheo cha Luteni Kanali, iwapo angeamua siku moja kuvaa Gwanda za Jeshi basi asingeweza kuvaa za cheo chake (Luteni Kanali) bali angevaa kama alivyovalia Rais Magufuli kwa kuwa hadhi yake kama rais ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama.

Inaelezwa kuwa uvaaji wa magwanda ya kijeshi kwa ngazi ya Rais siyo jambo la kisheria na hivyo lilazimishe ama kunyambulisha masharti ikitokea mkuu wa nchi anataka kuyatumia na kwa vile jeshi letu halijawahi kubuni cheo cha Amiri Jeshi Mkuu alichonacho rais, kwa kuwa kimafunzo na kitaratibu cheo kikuu cha mwisho ndani ya Jeshi letu ni Generali basi viongozi hao wakilazimika kuwa hivyo huvalia gwanda zisizo na cheo.

Wakielezea gwanda alilovaa Rais wa Kenya Uhuru Kenyetta, walisema cheo kinachoonekana kinatafsiri ya cheo cha ‘Field Marshall’ ambacho kwa taratibu za kijeshi hutunukiwa baada ya kuwa amepiganisha vita nyingi na kuwa bingwa wa utaalam wa medani za kivita.

Waliongeza kuwa Rais Yoweri Museven wa Uganda yeye ni Mwanajeshi mwenye Cheo cha U-Jenerali hivyo kubainisha kuwa, kwake kuvaa gwanda lenye vyeo hivyo ni sahihi.

Mv VictoriaMWANZA: Serikali imeendelea kutumbua majipu ya Ufisadi zamu hii ikiwakumba Kampuni ya Huduma za Meli (MSC) mkoa wa Mwanza baada ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kumsimamisha kazi Kaimu Meneja Mkuu Fabian Mayenga kwa ubadhirifu wa Sh milioni 600.

Mbali na Kaimu Meneja Mkuu, wengine waliosimamishwa ni kwa kuhusika na ubadhirifu huo, wengine ni Mwanasheria  Josephath Mushumbusi,  Kaimu Meneja Manunuzi, Abdallah Rumila pamoja na Meneja Miradi Alex Mchauru.

Prof. Mbarawa alisema hatua hiyo imefikiwa ili kupisha uchunguzi wa kina kwa tuhuma zinazowakabili huku akiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa kushirikiana na bodi  kuchunguza matumizi ya fedha na matengenezo ya Mv Butiama na Mv Victoria.

Fabiani Mayenga alianza kukaimu nafasi hiyo Desemba 26, mwaka 2014 baada ya aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe kumsimamisha kazi Meneja Mkuu Projestus Kaija kwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha.

Akieleza sababu za kusimamishwa kwao, Prof. Mbarawa alisema Serikali imefikia hatua hiyo kutokana na watumishi hao kutumia kiasi cha Sh milioni 600 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya matengenezo ya meli ya  Mv Victoria kulipana mishahara na meli hiyo kutokafanya kazi.

Alisema kosa lingine wanalotuhumiwa nalo ni kuichukua injini ya meli ya Mv Butiama na kuipeleka kutengenezwa kwa mtu ambaye alizuwia kutokana na kuidai mamilioni ya fedha huku wao wakiiandikia Serikali uongo kuwa injini hiyo ilikuwa haifai kutengenezwa wakijua ni nzima hivyo kuishauri serikali kununua injini mpya.

Kosa lingine ambalo aliwatuhumu nalo ni kuongeza thamani ya gharama za Bima za Meli na wakitafuna fedha iliyokuwa ikizidi na kujinufaisha wao wenyewe.

“Wametenda makosa makubwa na wala hawakustahili kuwa hapa, inasikitisha sana kwa umri wao kufanya mambo haya, hii itakuwa onyo kwa watumishi wengine na ninawaomba wale ambao hawawezi kazi na wapo hapa kwa ajili ya kujinufaisha waanze kuofungasha vilago mapemana kuondoka,” alisema.

Hata hivyo Prof. Mbarawa alisema serikali ipo katika mchakato wa kununua meli nyingine mpya kwa ajili ya kutoa huduma ya usafiri ndani ya ziwa Victoria kama ilivyokuwa imeahidiwa na Serikali awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete.

Meli ya Mv Victoria imesimama kutoa huduma ya usafiri katika mkoa wa Mwanza na Bukoba kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa kutokana na ubovu wa injini.

mahakama KuuTABORA: Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR – Mageuzi), amewasilisha pingamizi lake leo katika Mahakam Kuu Kanda ya Tabora akipinga ushindi aliopewa mgombea wa Chama Cha Mapindunzi (CCM) Hasna Mwillima.

Kafulila amewasilisha pingamizi hilo jana kupitia kwa wakili wake Daniel Lumenyela huku akiwa ameambatanisha nakala za fomu za matokeo ya kura ya vituo vyote 382 vya jimbo hilo ambazo zilisainiwa na mawakala wa CCM na kuonyesha kuwa mshindi iwapo zikijumulishwa.

Hata hivyo wakati akiwa mahakamani hapo kakamilisha taratibu za ufunguaji kesi, umati mkubwa wananchama wa vyama vinavyounda umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ulifurika tangu majira ya saa mbili asubuhi kama ishara ya kuonyesha kumuunga mkono na kumsindikiza Kafulila kupeleka madai yake hayo ya kesi.

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha pingamizi hilo, Kafulila alisema katika maombi yake kwa mahakama hiyo aliiomba mahakama ipitie nyaraka hizo na kisha imtangaze yeye kuwa ndiye mshindi wa uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Kusini.

Alidai msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo ambaye ni mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza Reuben Mfune alipewa shinikizo na viongozi wa Serikali amtangaze mgombea wa CCM Hasna Mwilima kuwa mshindi kwa kura zaidi ya 34,000 dhidi ya 32,000 alizopewa yeye.

Kafulila alisema kuwa toka siku hiyo Oktoba 28, mwaka huu yalipotangazwa matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo chini ya ulinzi mkali wa vyombo vya ulinzi na usalama msimamizi huyo bado hajaonekana hadharani.

Hata hivyo awali matokeo ya uchaguzi wa jimbo hilo yalikuwa yakitarajiwa kutangazwa Oktoba 27, mwaka huu na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo hilo lakini alitangaza kusitisha utangazaji huo kwa madai kuwa ameshauriwa na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kuagizwa kusitisha zoezi la utangazaji mpaka hapo baadaye.

Msimamizi huyo alikaririwa kuwa uamuzi wake huo wa kuwasiliana na ngazi za juu ulitokana na mgombea wa CCM Hasna Mwilima kugomea matokeo baada ya zoezi la kuhakiki kukamilika wakiwa na Kafulila.

“Haki ya wapiga kura wa Jimbo la Kigoma Kusini itapatikana lakini kinachofanyika ni kunichelewesha kunitangaza mimi kuwa mbunge,”  alisema Kafulila.

Alibainisha katika kile kinachoonyesha ni kuficha unyanganyi waliofanya hata nakala za majumuisho ya matokeo ya kura za wagombea hawakupewa wala kuonyeshwa fomu zake.

Kwa upande wake Wakili Lunyemela anayemwakilisha Kafulila katika shauri hilo alisema kuwa uchaguzi mzima haukuwa na utata na ndiyo maana mteja wake anadai mahakamani kutangazwa kuwa ndiye mshindi halali wa jimbo hilo.

"Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo alichofanya ni kuchukua matokeo ya kura ya mteja wake na kumpa aliyekuwa mgombea wa CCM Hasna Mwillima na ndiyo maana walilazimisha kuwepo kwa ulinzi mkali ili watangaze matokeo batili,” alisema.

Lunyemela alisema sheria ya uchaguzi na 343 imeweka vigezo muhimu vya kumpata na kumtangaza mshindi wa uchaguzi ikionyesha wazi kuwa aliyepata kura nyigi ndiye anastaili kuwa mshindi.

Akitangaza matokeo hayo, Msimamizi wa Jimbo la Kigoma Kusini, Reuben Mfune alisema, Hasna Mwillima ndiye mshindi baada ya kupata kura 34,453 huku Mbunge aliyekuwa akitetea jimbo hili David Kafulila wa NCCR Mageuzi akitajwa kupata kura 33,382 na Nashon Bidyanguze wa TADEA akipata kura 6382.

Rais MagufuliDAR ES SALAAM: Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli , leo mchana amefanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kukutana na hali ya kumsikitisha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga katika ziara yake hiyo pia amechukua hatua za kuvunja Bodi ya Hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenziwa wa Hospitali hiyo ya taifa.

“Rais amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini. Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akitoa maelekezo yafuatayo:

​Rais amevunja Bodi ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambayo ilishamaliza muda wake na amemteua Prof. Lawrence Mseru , kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Muhimbili kuanzia kesho tarehe 10 Novemba, 2015.

Dkt. Hussein L. Kidanto ambaye ndiye anayekaimu hivi sasa, amehamishiwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Balozi Sefue pia amesema, Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo.

Tayari Wizara ya Fedha imetoa shilingi bilioni 3 kwa ajili ya kazi hiyo na kulipa madeni ya ukarabati wa mashine za uchunguzi wa magonjwa nchini. Hata hivyo Katibu Mkuu Kiongozi amesema kuanzia sasa hospitali zote nchini zinatakiwa kutenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote (Regular Maintenance).

Balozi Sefue pia metumia nafasi hii kuwaagiza watendaji na viongozi wote katika sehemu za kazi kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na kazi za umma zinatekelezwa ipasavyo.

“Hakutakuwa na huruma kwa watumishi wa Umma wasiojali wananchi na mahitaji yao” Amesisitiza Balozi Sefue. Hii ni ziara ya pili ya kushtukiza ya rais Magufuli ambapo katika ziara yake ya kwanza alitembelea Wizara ya Fedha.